info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAZINDUA FAIBA MLANGONI KWAKO AWAMU YA PILI, WATEJA 400,000 KUNUFAIKA

Na Emerco Mashelle

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua rasmi utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako (FTTH), hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma ya intaneti ya kasi kwa wananchi, taasisi za umma na binafsi pamoja na wafanyabiashara kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Uzinduzi wa mradi huo umefanyika leo, Agosti 21, 2026, katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, CPA Moremi Marwa, amesema awamu ya pili ya mradi huo imelenga kuwafikia Watanzania wengi zaidi kwa kuwapatia huduma ya intaneti ya kasi kupitia mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao ni muhimu katika kuendesha shughuli za kijamii, kiuchumi na kibiashara.

Amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza mwezi Julai 2026, ambapo TTCL imeanza maandalizi na ujenzi wa miundombinu itakayowezesha huduma ya Faiba Mlangoni Kwako kufika katika maeneo mengi zaidi nchini.

“Utekelezaji wa mradi huu tayari umeanza mwezi Julai 2026. Katika hatua hii tunalenga kujenga takribani Home Pass 400,000,” amesema Marwa.

Ameeleza kuwa baada ya hatua hiyo, TTCL inalenga kuongeza idadi ya maeneo yatakayoweza kufikiwa na huduma hiyo hadi kufikia takribani Home Pass 750,000 ifikapo Juni 2027, na hatimaye kufikia Home Pass milioni moja ifikapo Juni 2028 baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa awamu hiyo ndani ya miaka mitatu.

Kwa mujibu wa Marwa, ongezeko la mahitaji ya huduma za mawasiliano, hususan matumizi ya intaneti katika maeneo ya makazi, taasisi, ofisi na biashara, limeifanya TTCL kuongeza kasi ya uwekezaji katika miundombinu ya kidijitali ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.

Amesema upanuzi wa huduma hiyo utasaidia wananchi kupata muunganisho wa intaneti wenye kasi na uhakika, sambamba na kuunga mkono azma ya Serikali ya kujenga uchumi wa kidijitali na kuongeza matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma mbalimbali.

“Huduma ya fiber ni sehemu ya mkakati wa TTCL wa kuboresha upatikanaji wa mawasiliano na kuwezesha matumizi mapana ya teknolojia katika elimu, biashara, taasisi na maisha ya kila siku ya Watanzania,” amesema.

Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako ni sehemu ya juhudi za TTCL katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini na kuchochea matumizi ya huduma za kidijitali, ukiwa unalenga kufikisha huduma za intaneti yenye kasi na uhakika katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.

 

Kukamilika kwa Awamu ya Pili ya Mradi wa Faiba Mlangoni Kwako kunatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kupanua wigo wa huduma ya intaneti ya kasi nchini, huku TTCL ikiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha Tanzania inakuwa na miundombinu imara ya mawasiliano kwa ajili ya maendeleo ya kidijitali.