TTCL YAZINDUA MSIMU WA BURE KABISA KWA WATEJA WA HUDUMA YA FAIBA MLANGONI KWAKO
Na Emerco Mashelle
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua rasmi zoezi la utoaji wa simu za mezani bila malipo ya ziada kwa wateja wa huduma ya Faiba Mlangoni Kwako (FTTH) wanaotumia vifurushi vya Shilingi 70,000 na kuendelea, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Shirika wa kuongeza thamani ya huduma na kuboresha uzoefu wa wateja.
Uzinduzi huo umefanyika Oktoba 28, 2026, katika Kituo cha TTCL Kijitonyama, Dar es Salaam, na kuongozwa na Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Bw. Vedastus Mwita, ambaye amesema maboresho hayo yanaonesha dhamira ya Shirika ya kuendelea kubuni huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja na kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bw. Mwita amesema kupitia maboresho hayo, wateja wa Faiba Mlangoni Kwako wanaolipia vifurushi vya Shilingi 70,000 na kuendelea watanufaika na huduma ya simu za mezani bila gharama ya ziada, hatua inayolenga kuongeza thamani ya huduma wanazopata kupitia kifurushi cha *T-Fiber Triple Hub*.
Ameeleza kuwa TTCL inaendelea kufanya maboresho ya huduma na vifurushi vyake ili kuhakikisha wateja wanapata suluhisho za mawasiliano zinazokidhi mahitaji yao ya kila siku, huku wakifurahia urahisi na thamani zaidi ya fedha wanazolipia.
“Lengo letu ni kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma zaidi kupitia kifurushi chetu cha T-Fiber Triple Hub, huku wakinufaika na urahisi na thamani ya huduma wanazolipia,” amesema Bw. Mwita.
Aidha, amesema huduma ya simu za mezani ina umuhimu mkubwa katika kurahisisha mawasiliano ya kifamilia, kijamii na kibiashara, ambapo itawawezesha wateja kuwasiliana kwa urahisi na wanafamilia, ndugu, marafiki pamoja na washirika wao wa biashara.
Kwa upande wa wafanyabiashara wadogo na wa kati, huduma hiyo inatarajiwa kuwa nyenzo muhimu ya kurahisisha mawasiliano na wateja, wafanyakazi na washirika wa biashara, hivyo kuchangia kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kila siku.
Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa TTCL itaendelea kutumia uzoefu wake wa muda mrefu katika sekta ya mawasiliano, pamoja na miundombinu ya kisasa ya Faiba Mlangoni Kwako, kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, nafuu na zinazokwenda sambamba na mahitaji ya sasa ya kidijitali.
Amesema maboresho hayo yanaendelea kuimarisha nafasi ya TTCL kama mtoa huduma muhimu wa mawasiliano nchini, huku Shirika likijikita katika kuongeza ubunifu, kuboresha huduma na kuhakikisha wateja wanapata thamani zaidi.
Katika hatua nyingine, Bw. Mwita amewahimiza wateja wa Faiba Mlangoni Kwako kutumia fursa hiyo kwa kuchagua vifurushi vya Shilingi 70,000 na kuendelea ili waweze kunufaika na huduma ya simu za mezani bila malipo ya ziada.
Pia, amewakaribisha wananchi ambao bado hawajaanza kutumia huduma ya Faiba Mlangoni Kwako kutembelea tovuti rasmi ya TTCL na kujisajili ili waweze kufikiwa na kuunganishiwa huduma hiyo katika maeneo yenye miundombinu husika.
Ameongeza kuwa TTCL itaendelea kusikiliza maoni na mahitaji ya wateja wake ili kuboresha huduma na kuhakikisha zinakidhi matarajio yao.
Aidha, TTCL inaendelea na jitihada za kuimarisha huduma za mawasiliano, kuongeza thamani kwa wateja na kuchochea matumizi ya teknolojia ya kidijitali kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.