info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

UBUNIFU, WELEDI, KUJITAMBUA NA KUJIAMINI VYA TAJWA KUWA SILAHA YA WANAWAKE KUTIMIZA MALENGO

Wanawake Wafanyakazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania wameshauri kuendeleza jitihada zaidi na ubunifu, kujitambua, kujiamini na weledi katika kutimiza malengo na kuleta mabadiliko katika nchi.

Aidha wamehimizwa kutosubiri kuwezeshwa bali watumie fursa zilizopo kujiwezesha huku wakitanguliza kujiamini katika majukumu yao ili kuongeza tija katika maendeleo ya Taifa. 

Ushauri huo ulitolewa  na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Bi. Zuhura Snare Muro alipokuwa akizungumza na wanawake hao ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Bi. Zuhura aliwataka wanawake hao kutosubiri kuwezeshwa bali watumie uwezo walionao kuongeza ubunifu na kufanya kazi kwa bidii.

" Asilimia tisini ya kile mwanamke unachoweza ni jitihada zako mwenyewe hizo nyingine zilizobakia ni kuongezewa nguvu tuu," alisema na kuongeza kuwa wanawake ni kundi la watu walio jasiri katika kila jambo jmbo la msingi ni kuondoa uoga katika kazi na majukumu wanayopewa.

Kwa upande wake, Mhandisi, Leticia Tinkas aliwashauri wanawake hususani waliopo katika kada ya uhandisi kuongeza jitihada kwa kuwa wao ndiyo chachu ya ukuaji wa Tehama na maendeleo nchini.

" Tunawapa moyo wanawake mbalimbali walioko idara za uhandisi hata wanafunzi walioko  shuleni waendelee na jitihada zaidi za kibunifu ili kutimiza malengo na kuleta mabadiliko katika nchi.

Mkurugenzi wa sheria, Bi. Anitha Moshi aliwahimiza wanawake kutambua Mawasiliano yao yako katika hali gani kuanzia ngazi ya jamii na hata kwa wale wanaofanya nao kazi kwani mawasiliano ni chachu ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo.

Alisema wanawake wa Shirika la Mawasiliano wanapaswa kuhakikisha wanaimarisha Mawasiliano katika sehemu za kazi hususani kwa wateja wao kwani ndio msingi wa ukuzaji wa uchumi.