UJUMBE WA UETCL WAPONGEZA TTCL KWA KUKUZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA KIDIJITALI AFRIKA MASHARIKI
Ujumbe kutoka Kampuni ya Kusafirisha Umeme nchini Uganda (Uganda Electricity Transmission Company Limited - UETCL) umetembelea Kijitonyama FTTx Experience Centre na kupongeza juhudi za Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika kuwekeza kwenye miundombinu na suluhisho za kidijitali zinazochangia maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.
Wakati wa ziara hiyo, Wajumbe walipata fursa ya kujionea teknolojia mbalimbali za kisasa zinazotolewa na TTCL kupitia Kijitonyama FTTx Experience Centre, ikiwemo huduma za intaneti za kasi, suluhisho za mawasiliano ya kidijitali na mifumo bunifu inayolenga kukidhi mahitaji ya wateja wa nyumbani, taasisi na biashara.
Ujumbe huo ulieleza kuvutiwa na uwekezaji uliofanywa na TTCL kupitia kituo hicho, ambacho kinatoa jukwaa la kuonesha uwezo wa teknolojia za kisasa na mchango wa Shirika katika kuimarisha mawasiliano ndani na nje ya mipaka ya Tanzania. Aidha, walibainisha kuwa TTCL imeendelea kuonesha uwezo mkubwa wa kuhakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana kwa ufanisi na kuendana na mahitaji ya uchumi wa kidijitali.
“Kituo hiki kinaonesha dhamira ya TTCL katika kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa na kuhamasisha ubunifu unaochangia maendeleo ya kidijitali katika ukanda wa Afrika Mashariki,” walieleza wajumbe hao.
Aidha, ujumbe huo ulitaja Kijitonyama FTTx Experience Centre kuwa ni kitovu cha ubunifu wa kidijitali (Innovation Hub) kinachoakisi maono ya TTCL ya kuongoza katika utoaji wa suluhisho za mawasiliano na teknolojia za kisasa. Walisisitiza kuwa uwepo wa kituo hicho unaimarisha juhudi za kukuza matumizi ya teknolojia, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kuharakisha mabadiliko ya kidijitali katika taasisi na jamii kwa ujumla.
Kupitia ziara hiyo, TTCL imeendelea kuonesha nafasi yake kama mdau muhimu katika maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano na teknolojia nchini, huku ikiimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukuza uchumi wa kidijitali na ubunifu wa kiteknolojia.