info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

VIONGOZI WA TAASISI NA MASHIRIKA WAPEANA UZOEFU KUBORESHA UTENDAJI KAZI

Wenyeviti wa Bodi na Wakuu wa Taasisi za Umma wameendelea na Kikao Kazi kilichowakutanisha jijini Arusha kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Taasisi na Mashirika wanayoyaaimamia

Mkurugenzi Mkuu wa TTCL CPA Moremi Marwa ni miongoni wa Viongozi kutoka Taasisi na Mashirika ya Umma 248 yaliyopo jijini Arusha katika Kikao muhimu kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Kikao Kazi hiki kilichofunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kinatarajiwa kumalizika Agosti 30 Mwaka huu.

Majadiliano mbalimbali katika katika Kikao hicho yanalenga kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati mipya ya kuboresha utendaji wa taasisi hizo ili kuendana na maelekezo ya serikali ya kuleta ufanisi na tija zaidi katika sekta ya umma.

Aidha Viongozi hawa walipata fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu changamoto zinazowakabili, namna ya kuzitatua, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika taasisi wanazoongoza. 

Kupitia mawasilisho na mijadala ya kina, viongozi wamejadili mbinu bora za usimamizi, namna ya kukabiliana na changamoto za kifedha, na mikakati ya kuimarisha ufanisi wa taasisi zao.

Moja ya masuala makuu yaliyosisitizwa ni umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa taasisi za umma. Viongozi walihimizana kuhakikisha kwamba wanaimarisha mifumo ya ndani ya udhibiti na kutoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa mamlaka husika, ili kuepuka upotevu wa rasilimali za umma. 

Aidha, walitakiwa kuimarisha uhusiano na wadau mbalimbali ili kuhakikisha kuwa taasisi zao zinapata msaada wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu yao.

Viongozi walikubaliana kwamba kuna umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii, kuwa wabunifu, na kutumia teknolojia za kisasa ili kufikia malengo ya taasisi zao na serikali kwa ujumla.

Kikao hiki kilidhihirisha umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa viongozi wa taasisi za umma, na kinaonekana kuwa hatua muhimu kuelekea kuimarisha utendaji na kuongeza uwajibikaji katika sekta ya umma nchini.