info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WAFANYAKAZI WA TTCL MKOA WA PWANI WAJENGEWA UWEZO KUHUSU TEKNOLOJIA ZA FTTX

Wafanyakazi wa TTCL Mkoa wa Pwani, wakiongozwa na Meneja wa Mkoa, Bw. Abdulrahim Chotta, wametembelea Kijitonyama FTTx Experience Centre kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuongeza uelewa kuhusu teknolojia za kisasa za mawasiliano zinazotolewa na Shirika.

Ziara hiyo imefanyika tarehe 3 Juni 2026 ikiwa ni sehemu ya jitihada za TTCL za kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wake ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za biashara na huduma za mawasiliano.

Wakiwa katika kituo hicho, Wafanyakazi hao walipata fursa ya kujionea kwa vitendo namna huduma za Faiba Mlangoni Kwako (FTTx) zinavyotekelezwa, kuanzia hatua za ufungaji wa huduma hadi matumizi ya teknolojia mbalimbali zinazowezesha utoaji wa intaneti yenye kasi, ubora na uhakika kwa wateja wa makazi na taasisi.

Aidha, walijifunza kuhusu ubunifu na suluhisho za kidijitali zinazotumiwa na TTCL katika kuimarisha uzoefu wa wateja na kuhakikisha huduma za mawasiliano zinakidhi mahitaji ya uchumi wa kidijitali unaokua kwa kasi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja wa Mkoa wa Pwani, Mwl. Abdulrahim Chotta, alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uelewa wa wafanyakazi kuhusu huduma za FTTx na kuwajengea uwezo wa kuzitangaza na kuzisimamia kwa ufanisi zaidi katika maeneo yao ya kazi.

Ziara hiyo imeonesha dhamira ya TTCL ya kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu, kukuza utamaduni wa kujifunza na kubadilishana uzoefu, pamoja na kuhakikisha watumishi wanakuwa na uelewa wa kina wa teknolojia na huduma zinazotolewa na Shirika.