WAJUMBE WA BODI YA WAKURUGENZI TTCL WAJIONEA MAFANIKIO YA HUDUMA NA UBUNIFU WA KIDIJITALI SABASABA 2026
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) watembelea Banda la TTCL katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), ambapo wamejionea maendeleo ya huduma na suluhisho mbalimbali za kidijitali zinazotolewa na Shirika kwa wananchi, taasisi za umma, sekta binafsi na wafanyabiashara.
Katika ziara hiyo iliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, wajumbe wa Bodi walipokea maelezo kuhusu huduma mbalimbali za TTCL zinazochangia kuimarisha mawasiliano na kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.
Miongoni mwa huduma walizojionea ni Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), huduma za Faiba Mlangoni Kwako, TTCL Public Wi-Fi, Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (National Internet Data Centre – NIDC), pamoja na suluhisho za biashara zinazowezesha taasisi na kampuni kutumia teknolojia za kisasa katika utoaji wa huduma.
Wajumbe wa Bodi pia walitembelea FTTx Experience Centre, ambapo walijionea matumizi ya teknolojia ya intaneti ya nyuzi macho (Fiber to the Home) katika kuwezesha huduma za nyumba mahiri (Smart Home) na suluhisho nyingine za kidijitali zinazorahisisha maisha ya kila siku.
Ziara hiyo ilitoa fursa kwa Wajumbe hao kujionea namna TTCL inavyoendelea kutekeleza dhamira yake ya kutoa huduma za mawasiliano zenye ubora, salama na za uhakika kupitia uwekezaji katika miundombinu ya kisasa na teknolojia bunifu.
Kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, TTCL inaendelea kuunganisha mikoa ya Tanzania na nchi jirani kwa miundombinu ya kisasa ya mawasiliano, huku huduma za Faiba na suluhisho nyingine za kidijitali zikiwezesha wananchi, taasisi na wafanyabiashara kunufaika na intaneti ya kasi ya juu na huduma zinazochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.