info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

WATAALAMU WA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KUTOKA KOREA WAPONGEZA UWEKEZAJI WA TTCL KATIKA TEKNOLOJIA YA KISASA YA NIDC

Na Spencer Julius

Wataalamu kutoka Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (Korea International Cooperation Agency – KOICA) wamelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa uwekezaji wake katika miundombinu ya kisasa ya teknolojia inayopatikana katika Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).

Pongezi hizo zimetolewa na Bw. Dongmin Kim, Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari (IT Specialist) kutoka Korea, anayehusika na Mradi wa Kituo cha Afya ya Kidijitali (Center for Digital Health Project), wakati wa ziara ya wataalamu hao katika kituo cha NIDC. Ziara hiyo ilikuwa na lengo la kujifunza na kufahamu namna kituo hicho kinavyoendesha shughuli zake, huduma zinazotolewa pamoja na mchango wake katika kukuza maendeleo ya teknolojia ya kidijitali nchini.

 Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Dongmin Kim ametoa pongezi kwa TTCL kupitia NIDC kwa uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya TEHAMA, akieleza namna miundombinu hiyo ilivyo muhimu katika kuimarisha huduma za kidijitali na kusaidia utekelezaji wa miradi inayotegemea teknolojia.

 Wataalamu hao wamepokelewa na Meneja Biashara wa Kituo cha NIDC, Bi. Leila Masanga, ambaye amewapatia maelezo kuhusu shughuli mbalimbali zinazotekelezwa kituoni hapo, matumizi ya miundombinu ya kiteknolojia na fursa zinazopatikana kupitia huduma zinazotolewa na NIDC.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bi. Leila Masanga amewashukuru wataalamu hao kwa kutembelea kituo hicho na kupata fursa ya kujionea shughuli zinazofanyika. Amewahimiza kuwa mabalozi wazuri wa huduma zinazotolewa na NIDC kwa kuzitambulisha kwa watu na taasisi mbalimbali ili kuongeza uelewa na matumizi ya fursa zinazopatikana kituoni hapo.