info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

WAZIRI NAPE AMLILIA MAREHEMU KAPEMBE, AMPA TUZO YA KIHISTORIA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akabidhi tuzo kwa familia ya Marehemu Joachim Kapembe, kwa kutambua na kuthamini mchango wa Marehemu Joachim Kapembe wakati wa uzinduzi wa huduma ya Mawasiliano ya Intaneti katika kilele cha Mlima Kilimanjaro Disemba 13 2022. Waziri Nape amesema marehemu Joachim Kapembe ni miongoni mwa watu waliomtia nguvu, ujasiri na ari kuweza kufika katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro na kufanikisha uzinduzi wa huduma hiyo. “Joachim Kapembe ameacha alama ambayo itaendelea kukumbukwa na kuenziwa kwenye Taifa letu” ameongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe, Nape Moses Nnauye. Tuzo hiyo imetolewa katika hafla iliyofanyika Julai 22, mwaka huu Marangu Gate, Mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kutambua mchango wa wafanyakazi waliofanikisha ujenzi wa mawasiliano katika Mlima Kilimanjaro na walioshiriki uzinduzi wa huduma hiyo katika kilele cha mlima Kilimanjaro Disemba 13,2022. Marehemu Joackim kapembe alikuwa mfanyakazi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) na alifariki wakati wa kushuka mlima kilimanjaro wakati akiwa anawahisha taarifa za matukio aliyochukua wakati wa hafla ya kufikisha mawasiliano ya intaneti ya kasi katika kilele cha mlima huo tatehe 13 Disemba, 2022. Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Bi. Zuhura Sinare Muro amesema Taifa letu limepata pigo kwa kuondokewa Marehemu Kapembe na Shirika la Utangazaji Tanzania –TBC ambaye tulikuwa naye katika safari ya kuelekekea Kilele cha Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya uzinduzi na wakati wa safari alikuwa mchangamfu na mwenye kujituma muda wote. “Hakika tumepoteza mtu muhimu katika Taifa letu, mchango wake hautakuja kusahulika katika sekta ya Habari, Mawasiliano na Taifa kwa ujumla” ameongeza Bi, Zuhura Muro. Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa Shirika litaendelea kuenzi mchango wa Marehemu Joachim Kapembe, Mwandishi wa Habari na Mpigapicha wa Shirika la Utangazaji Tanzania- TBC kwa ujasiri na uzalendo mkubwa aliouonesha katika utekelezaji wa majukumu yake hasa aliposhiriki katika Uzinduzi wa huduma ya Intaneti Mlimani Kilimanjaro.