info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAPOKEA TUZO UIMARISHAJI WA UCHUMI WA KIDIJITALI NCHINI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemkabidhi tuzo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Moremi Marwa, ikiwa ni kutambua mchango mkubwa wa shirika hilo katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa hafla ya uzinduzi wa minara 758 ya mawasiliano, muunganisho wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika wilaya 85, pamoja na makabidhiano ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa Serikali.Tukio hilo muhimu lilifanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na wadau wa sekta ya TEHAMA.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Rais alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma bora, za uhakika na zenye gharama nafuu, sambamba na kuimarisha uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wake, TTCL ilieleza kuwa tuzo hiyo ni chachu ya kuongeza juhudi katika ubunifu, ufanisi wa huduma na utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga kupanua upatikanaji wa mawasiliano nchini.

Aidha, katika hafla hiyo, TTCL ilipokea rasmi Hati ya Makabidhiano ya uendeshaji wa miundombinu ya mawasiliano iliyojengwa kwa ushirikiano wa watoa huduma za mawasiliano (Consortium of Mobile Operators). Hati hiyo ilikabidhiwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, na kushuhudiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Makabidhiano hayo yanaashiria hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa miundombinu ya mawasiliano nchini, huku TTCL ikiendelea kuchukua nafasi ya kipekee katika kuunganisha Taifa na kuendeleza ajenda ya Tanzania ya kidijitali.